
BAADA ya kipigo cha msimu cha bao 6-2 kutoka kwa klabu ya Yanga wiki iliyopita, Kagera Sugar wameendeleza rekodi yao ya kupigwa katika dimba la Kaitaba baada ya leo kukubali kichapo cha goli 3-2 toka kwa wanalambalamba, timu ya Azam FC.
Kipindi cha kwanza kilianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu lakini kwa nidhamu ya hali ya juu na hivyo kusababisha ukame wa magoli kwenye kipindi hicho.
Ukame huo ulikatwa na mshambuliaji mkongwe, Temi Felix dakika ya 32 baada ya kuukwamisha mpira wavuni akiunganisha kross iliyopigwa toka upande wa kulia na kumshinda Aishi Manula.
Hata hivyo bao la Temi Felix halikudumu kwani kiungo wa Azam, Mudathir Yahya alisawazisha bao hilo dakika ya 40 na hivyo kufanya timu hizo kwenda mapumziko kwa sare ya bao 1-1
Baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, iliwachukua Kagera Sugar dakika 68 na kupachika bao la uongozi kwa mkwaju wa penalti kupitia kwa Temi Felix.
Ndoto za Azam kupata pointi 3 zilianza baada ya sub ya Jean Baptist Mugiraneza na nafasi yake kuchukuliwa na Domayo aliyepachika mpira wavuni dakika ya 80.
Matumaini yalifufuka kama utani baada ya nahodha John Bocco kuudumbukiza mpira nyavuni dakika za mwisho na hivyo kupeleka chereko hizo katika viunga vya Chamanzi.
Kwa ushindi huo Azam wanafufua matumaini ya kuwania taji la VPL wakikwea hadi nafasi ya nne huku wakiwamwaga Mtibwa pamoja na na Kagera Sukari.
Post a Comment