
KIKOSI cha
Simba kilichokwenda mkoani Dodoma kujiweka sawa kwa ajili ya michezo ijayo ya
Ligi Kuu Bara, kimerejea jijini Dar es Salaam jana Jumapili kwa ajili ya
kuendelea na ratiba ya VPL.
Simba ilikwenda mkoani humo baada ya
kupata mwaliko wa kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Polisi Dodoma inayoshiriki
Ligi Daraja la Kwanza na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Hata hivyo, kocha msaidizi wa timu
hiyo, Mganda, Jackson Mayanja, amesema kwamba kupata safari hiyo pamoja na
kucheza mchezo huo wakati ligi kuu imesimama, imekuwa ni faida kubwa kwao
katika kujiweka sawa na kurekebisha waliyoyaona katika mechi zao mbili za
awali, hivyo sasa wamekuwa fiti zaidi katika kila sekta.
“Mazoezi na mechi tuliyocheza Dodoma
imekuwa na mchango mkubwa kwa maandalizi na kujiweka fiti zaidi kwa ajili ya
michezo inayokuja, imekuwa vyema kupata nafasi ya kuja sehemu kama hii wakati
ligi imesimama na kupata muda wa kurekebisha tuliyoyaona kwenye mechi za awali
za ligi.
“Bado safari ni ndefu na ligi ina
mechi nyingi, kwa hiyo unapopata nafasi kama hii na unapoitumia vizuri, inaleta
faida kubwa kwa mechi za baadaye, ukizingatia msimu huu tunahitaji kufanya
vizuri zaidi,” alisema Mayanja.
Mpaka sasa, Simba imecheza mechi
mbili za ligi, ya kwanza waliumana na Ndanda na kushinda kwa mabao 3-0, mechi
ya pili wakatoka suluhu dhidi ya JKT Ruvu, jumla imekusanya pointi nne.
Keshokutwa Jumatano wanatarajia kucheza dhidi ya Ruvu Shooting.
Post a Comment