![]() |
Picha na Zubery. |
TIMU ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Tanzania imefuzu hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania tiketi ya Fainali za Afrika mwakani Madagascar, baada ya kuifunga Afrika Kusini mabao 2-0 jioni ya leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Serengeti boys imeibuka kwa jumla ya ushindi wa magoli 3-1 baada ya kulazimisha sare ya goli moja kwa moja kwenye mchezo wa awali uliofanyika huko Africa Kusini.
Magoli ya Serengeti Boys yaliwekwa kimiani a Mohamed Rashid Abdallah katika kipindi cha kwanza na Muhsin Malima Makame kipindi cha pili.
Pamoja na ushindi huo, Tanzania maarufu kama Serengeti Boys ililazimika kucheza pungufu tangu dakika ya 44 baada ya kiungo wake wa ulinzi, Ally Hamisi Ng’anzi kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa kwa kadi nyekundu.
Serengeti Boys ilipata bao lake la kwanza dakika ya 34 baada ya Mohamed Rashid Abdallah kumalizia vizuri pasi ya Yohana Nkomola kumtungua kipa wa Amajimbos Glen Tumelo Baadjes.
Benchi la Ufundi la Serengeti Boys, chini ya Mkurugenzi wa Ufundi, Mdenmark Kim Poulsen, Kocha Mkuu, Bakari Shime na Kocha wa makipa, Muharami Mohammed ‘Shilton’, lilirudi na mipango mizuri kipindi cha pili na timu ikaendelea kutawala mchezo licha ya kucheza pungufu.
Kipindi cha pili kilianza kwa vijana wa Serengeti Boys kucheza kwa kujihami baada ya kuwa pungufu, lakini bado haikuzuia kitu kwa vijana hao waliokuwa na uchu wa magoli a ndipo dakika ya 83, Muhsin Malima Makame akakwamisha wavuni goli la pili na la ushindi la kuzima matumaini ya Africa Kusini kusonga mbele.
Ushindi wa Serengeti Boys unawafanya kufuzu katia hatua ya tatu na hivyo kumsubiri mshindi kati ya Congo au Namibia.
Post a Comment