
KLABU ya Azam imeibuka
kidedea kwa kuichapa jumla ya penalty 4-1 katika mchezo wa ngao ya jamii wa
kuukaribisha msimu mpya wa ligi wa 2016-2017 baada ya dakika 90 kumalizika kwa
sare ya goli 2-2.
Yanga ambao walikuwa wakiishikilia Ngao ya Jamii baada ya
kuifunga Azam kwenye mchezo wa msimu uliopita kwa changamoto ya mikwaju ya
penati, walikuwa kwenye nafasi nzuri ya kubeba tena ngao hiyo kutokana na
kuongoza mchezo huo kwa magoli 2-0, magoli yaliyofungwa kipindi cha kwanza.
Mshambuliaji
wa Yanga Donald Ngoma alifunga bao la kwanza dakika ya 20 kwa njia ya penati
kufuatia yeye mwenyewe (Ngoma) kuanngushwa kwenye box na beki wa Azam David
Mwantika.
Dakika moja baadaye, Ngoma akaifungia tena Yanga bao la pili
akiunganisha pasi ya Amis Tambwe ambaye alitumia vizuri makosa ya Mwantika
aliyeshindwa ku-control mpira na kunyang’anywa na Tambwe.

Dakika 45 za kipindi cha kwanza zikamalizika kwa Yanga kuwa
mbele kwa mabao 2-0 dhidi ya Azam FC.
Dakika
ya 74 Shomari Kapombe aliipatia Azam bao la kwanza akitumia makosa ya mabeki wa
Yanga waliozembea kuondosha mpira kwenye eneo la hatari la goli lao.
John Bocco ‘Adebayor’ aliisawazishia Azam kwa mkwaju wa penati dakika ya
90 penati iliyotokana na beki wa Yanga kuushika mpira kwenye box

Deogratius Munishi ndiye mchezaji pekee aliyefunga penati kwa upande wa
Yanga huku Hassan Kessy akishuhudia penati yake ikidakwa na golikipa wa Azam
Aishi Manula wakati Haruna Niyonzima yeye penati yake iligonga ‘mtambaa panya’
na kutoka nje.
Katika kipindi cha miaka mitano ya hivi karibuni, Azam na
Yanga zimekutana mara nne mfululizo kuwania Ngao ya Jamii huku Yanga wakiongoza
kuinyakua mara nyingi zaidi ya wapinzani wao.
Yanga
wametwaa ngao hiyo mara tatu (mara zote kwa kuifunga Azam) huku ushindi wa leo
ukiwapa Azam ngao hiyo kwa mara ya pili.
Post a Comment