![]() |
picha na shaffih |
Yanga imeshindwa kutamba kwa mara nyingine tena kwenye uwanja wa nyumbani
baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Medeama SC ya Ghana
katika mchezo wa Kundi A michuano ya kombe la Shirikisho Afrika.
Donald Ngoma alianza kuifungia Yanga bao la kuongoza dakika ya pili ya
mchezo huo akitumia vema makosa ya safu ya ulinzi ya Medeama na kuiweka timu
yake mbele ya Medeama kwa bao 1-0.
Dakika 15 za kwanza watoto wa Jangwani walitawala mchezo kwa pasi za haraka
huku wakiliandama lango la Medeama kitendo kilichosababisha wapate kona kadhaa.
Medeama walisawazisha bao hilo dakika ya 17 baada ya Bernard Danso
kuunganisha mpira wa kona na kufanya matokeo kuwa 1-1 ambayo yalidumu hadi
dakika 90 zinamalizika.
Mechi ya leo ilikuwa ni muhimu kwa vijana wa Hans van Pluijm kupata
ushindi ambao ungewapa pointi tatu na kunyanyua morali ya kufanya vizuri kwenye
kundi lao.
Yanga inaendelea kusalia katika nafasi ya mwisho kwenye kundi lake ikiwa
na pointi moja baada ya kucheza mechi tatu bila ushindi huku ikiwa imepoteza
mechi mbili. Yanga ilifungwa goli 1-0 ugenini na MO Bejaiya ya Algeria kwenye
mchezo wa kwanza wa Kundi A kabla ya kukubali kichapo kingine kwenye uwanja
wake wa nyumbani dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo.
Medeama yenyewe inasalia kwenye nafasi yake ya pili kwa pointi zake
mbili baada ya kucheza mechi tatu, ilifungwa 3-1 kwenye mechi ya kwanza dhidi
TP Mazembe kisha ikatoka suluhu na MO Bejaia. Mazembe inaendelea kuongoza kundi
hilo ikiwa na pointi sita mbele ya Bejaia yenye pointi nne kabla timu hizo
hazijakutana zenyewe kwa zenyewe kwenye mchezo wa kesho.
Post a Comment