
Antoine
Griezmann ameshinda kiatu cha adhabu kwenye Michuano ya Euro mwaka huu baada ya
kufunga magoli sita na kutoa assist mbili ndani ya dakika 555 alizocheza.
Cristiano Ronaldo na Olivier Giroud wamemaliza nafasi ya pili na ya tatu
mtawalia.
Hata hivyo, Griezmann (25) na timu yake ya Ufaransa jana
walikuwa na huzuni kubwa baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Ureno
na amesema kwamba tuzo hiyo haina maana yoyote kwake kutokana na timu yake
kukosa ubingwa ambao wao ndio walikuwa waandaaji wa mashindano hayo.
Mchezaji huyo wa Atletico Madrid amekuwa moja ya
wachezaji mahiri kwenye michuano ya mwaka huu, lakini nafasi zake mbili
alizopata kwenye mchezo wa jana hazikuweza kuzaa matunda. Griezmann amesema
zawadi hiyo pengine ataisherehekea baadaye.
“Kuna ukatili na faraja kwa wakati mmoja,” Griezmann
amesema. “Tumekuwa na wakati bora sana, lakini vile vile wakati wenye huzuni
kubwa. Tunapaswa kujifunza. Lakini usiku wa leo (jana) tumejitahidi kwa kila
namna na hatujutii kwa hilo. Ninajivunia kikosi chetu na kila mmoja wetu.
Kilichobaki kwa sasa ni kupumzika na kuja na nguvu mpya.
“Safari hii tumeshindwa kufurukuta tofauti na ilivyokuwa
dhidi ya Ujerumani. Kiukweli inauma sana. Tumepiga miamba, nilipata nafasi pia
na ilibaki kidogo tu nifunge. Kipa akafanya kazi yake vyema. Inahuzunisha sana,
lakini hakuna jinsi zaidi ya kujipanga na kurudi na nguvu mpya.”
Na alipoulizwa kama anajivunia kushinda tuzo ya ufungaji
bora, Griezmann alisema kamwe hawezi kuwa na furaha nayo kwa sasa hasa baada ya
kuona timu yake ikipoteza na badala yake amesema muda huu akili yake yote ipo
kwenye timu.
“Labda kwa baadaye ndiyo naweza kuihisi hii tuzo, lakini
kwa sasa hapana. Lazima kwa pamoja wachezaji wote tuwe na huzuni. Napatwa na
huzuni kubwa nikiwaangalia wachezaji wenzangu. Nilitaka kutoa mchango wangu
kubakisha taji hili hapa. Lakini ndiyo hivyo imeshindikana hakuna namna tena.”
Post a Comment