UONGOZI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati
Azam FC, umetangaza rasmi kuwatema wachezaji sita kwa awamu ya kwanza huku
nyota wawili wakifeli majaribio.
Nyota hao walioachwa ni makipa Ivo Mapunda, Khalid
Mahadhi aliyekuwa ametolewa kwa mkopo Mafunzo ya Zanzibar, mabeki Said Morad,
Racine Diouf kutoka Senegal pamoja na washambuliaji Didier Kavumbagu (Burundi)
na Allan Wanga (Kenya).
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Ofisa Habari wa Azam FC,
Jaffar Idd, alisema wachezaji hao wameachwa wakiwa wamepata stahiki zao kwa
wale ambao waliokuwa wamebakiwa na mikataba.
Alisema mbali na wachezaji hao, pia wachezaji
wawili kati ya wanne waliokuwa kwenye majaribio nao wameachwa rasmi ambao ni
beki wa kushoto kutoka Ghana, Nurudeen Yusif aliyetokea Medeama ya huko na
kiungo mshambuliaji David Wirikom (Cameroon).
Wawili hao wamepewa majibu ya kufeli majaribio yao
leo asubuhi [juzi] kufuatia Kocha Mkuu Zeben Hernandez, kutoridhishwa na uwezo
wao kwa siku nne walizofanya mazoezi na kikosi cha Azam FC.
“Wakati tunajiandaa na msimu mpya kuna wachezaji
tuliwaalika kutoka nchi mbalimbali Afrika kwa ajili ya kufanya majaribio, ambao
mpaka sasa wapo wanne, tangu tulipoanza mazoezi kwa siku takribani nne mwalimu
leo ameamua kuwapunguza wawili na wawili wamebakia.
“Waliofeli majaribio ni David Wirikom kutoka
Cameroon na Nurudeen Yusif kutoka Ghana, kocha ameona viwango vyao
havitofautiani sana na viwango vya wachezaji wetu hapa nyumbani, kocha ameongea
nao leo mara baada ya mazoezi na kuwaambia haoni kama wanaweza kumsaidia kwa
sababu anataka kuona mtu wa kimataifa anayekuja awe zaidi ya wachezaji wetu,”
alifafanua msemaji wa klabu siku ya juzi..
Wachezaji wanaoendelea kwenye majaribio ni makipa
Daniel Yeboah (Ivory Coast) na Juan Jesus Gonzalez (Hispania), ambao wanawania
nafasi moja ya usajili katika eneo la golikipa.
Jaffar alimalizia kwa kusema kuwa wanatarajia
kuwapokea wachezaji wengine wa kimataifa ndani ya siku mbili au tatu zijazo kwa
ajili ya majaribio.
Post a Comment