
Mambo yanazidi Kuwa mambo
kwa mshambuliaji Thomas Ulimwengu baada ya kupata ofa nyingine ya dola milioni
1 (zaidi ya Sh bilioni 2.2).
Klabu kubwa zaidi barani Afrika ya Al Ahly ya Misri ndiyo imetoa
ofa hiyo kubwa ikimtaka Ulimwengu ambaye sasa ni mchezaji huru ajiunge nayo.
Said El Amry, mmoja wa mawakala wanaofanya kazi na Al Ahly
katika suala la kusaka wachezaji ameliambia Championi kuwa Ahly wako tayari
kumwaga kitita hicho katika mafungu mawili.
“Tumefanya mazungumzo na wakala wake, lakini hatujajua kama
amekubali. Inaonekana ni kama hamsini kwa hamsini. Maana ametuambia bado kuna
timu za Ulaya pia zinamhitaji,” alisema.
Juhudi za kumpata meneja wake Ulimwengu zilifanyika kwa siku
mbili hadi juzi alipozungumza na gazeti hili kusema wao wanataka kwanza kabisa
aende Ulaya.
“Kweli, tunajua Al Ahly inamhitaji Ulimwengu na kila kitu kipo
wazi. Lengo namba moja ni kwamba aende Ulaya na huo ndiyo mpango.
“Kuna timu za Ulaya zinamtaka na mazungumzo yameanza. Sisi
tumelenga zaidi Ulaya. Kuna Al Ahly, timu nyingine za Misri, pia ziko za Afrika
Kusini. Acha tuangalie Ulaya,” alisema Jamal Kisongo.
Tayari KRC Genk ya Ubelgiji ambayo anacheza Mbwana Samatta
imeonyesha nia ya kumtaka Ulimwengu ambaye aliamua kutosaini mkataba na TP
Mazembe.
SOURCE: CHAMPIONI
Post a Comment