
KOCHA wa timu ya taifa ya Algeria, maarufu kama mbeha wa jangwani, Milovan Rajevac amejiuzulu baada ya kuiongoza timu hiyo kwa michezo miwili pekee.
Maamuzi hayo yamekuja siku chache baada ya timu hiyo kulazimishwa sare ya goli 1-1 dhidi ya timu ya taifa ya Cameroon katika kundi B michuano ya kufuzu fainali za kombe la dunia za mwaka 2018 nchini Urusi.
Rajevac, 62, raia wa Serbia alikutana na rais wa shirikisho la mpira wa miguu la Algeria Mohamed Raouraoua siku ya jumanne kujadili mambo kadha wa kadha ikiwemo matokeo ya sare ya 1-1 na baadae ikatangazwa kuhusu kuondoka kwake muda mchache baada ya mazungumzo yale.
Rajevac alichukua nafasi ya Mfaransa Christian Gourcuff ambaye alibwaga manyanga mwezi April.
Algeria watakuwa na mchezo mwingine wa kufuzu fainali za kombe la dunia na timu ya Nigeria tarehe 12 ya mwezi November.
Timu itakayokuwa kinara wa kundi ndiyo itakuwa imekata tiketi ya fainali hizo zitakazofanyika nchini Urusi.
Shirikisho la nchi hiyo pia lilitangaza siku ya Jumanne lilituma ombi kwa FIFA ili kumpata kinda anayekipiga katika klabu ya Bordeaux, Adam Ounas ili kucheza timu ya taifa ya Algeria licha ya kucheza timu ya vijana ya Ufaransa ya chini ya miaka 20.
"Yalikuwa maamuzi ya moyo wangu, hivyo, ilikuwa ngumu sana kutenda kinyume na moyo wangu" Alisema kinda huyo alipokuwa akihojiwa na BBC RADIO 5.
Ounas alizaliwa Ufaransa na kukulia huko lakini anaweza kicheza Algeria kutokana na wazazi wake kuwa raia wa Algeria.
Post a Comment