
Zikiwa zimesalia takribani siku 14
ili kuanza kwa msimu wa ligi kuu ya soka Tanzania msimu wa 2016/2017, afisa
habari wa klabu ya wekundu wa msimbazi Simba Haji Manara amesema hatarajii
kuona mapungufu yaliyojitokeza kwenye msimu uliopita yaani 2015/2016.
Manara alizungumza mara baada ya
mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi Boniface Wambura kusema kwamba, msimu uliopita
waamuzi walijitahidi kusimamia sheria 17 za soka kwasababu hadi ligi
inamalizika hakuna mwamuzi aliyefungiwa kutokana na kuchezesha bila kufata sheria.
Kauli hiyo imepingwa na Manara
ambaye amesema, klabu ya Simba ilipeleka malalamiko yasiyopungua nane juu ya
maamuzi mabovu yaliyoihusha timu yao lakini hakuna lalamiko hata moja
lililofanyiwa kazi wala kujibiwa.
“Bodi ya ligi wamesema msimu
uliopita kulikuwa na ubora kwenye uamuzi, sisemi uongo lakini siyo kweli, msimu
uliopita kulikuwa na uvundo kwenye maamuzi. Simba tumelalamika karibu mechi
nane kwa kutuma malalamiko yetu kwa barua rasmi na hawakutoa maamuzi wala
kusema lolote. Kama wao waliona ligi ya mwaka jana ilikuwa na maamuzi mazuri,
itakuwa ni kituko,” alisema Manara.
Wakati huohuo Manara akasema hatarajii
pia kuona mambo kadhaa yaliyojitokeza wakati wa msimu uliopita yakijirudia
tena, timu kubadilisha kituo bila sababu za msingi wala timu kuruhusiwa kwenda
kushiriki mashindano yasiyo rasmi na kusababisha ligi kusimama.
“Ligi iliyopita ilikuwa na
changamoto nyingi mno, ilifika mahali timu inabadilisha kituo, ugenini inakuwa
nyumbani na nyumbani inakuwa ugenini hatupendi kuona haya mambo yanajitokeza
tena wala hatutarajii kuona vitu hivyo vinatokea,”
“Jambo hili lilitokea kwenye mechi
ya Yanga na Ndanda, halijawahi kutokea sehemu yeyote duniani tangu dunia
imeumbwa hatutarajii hilo jambo litokee tena. “
“Msimu uliopita ligi ilisimama
kupisha timu iliyokwenda kucheza bonanza, hatutarajii hayo yatokee tena
kwasababu hata hao wadhamini wanaotoa hela watachoka kwamba kila siku ligi
inamalalamiko. Hizi siyo changamoto ni matatizo kwa TFF na Bodi ya Ligi.”
Post a Comment