
SHIRIKISHO la
mpira wa miguu nchini, TFF limemchagua beki wa kati wa Simba, Method Mwanjale kuwa
mchezaji bora wa mwezi Desemba wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa msimu wa 2016/2017.
Beki huyo wa kati, aliwashinda
kiungo mshambuliaji wa Yanga, Haruna Niyonzima na beki Yakubu Mohamed wa Azam
FC. Mwezi Desemba ulichezwa raundi tatu za Ligi hiyo, huku Simba ikicheza mechi
mbili ugenini na moja nyumbani. Raundi hizo ni ya 16, 17 na 18.
Mwanjali aliiongoza Simba
kushinda mechi zote tatu, hivyo timu yake kupata ushindi wa asilimia 100 kwa
kunyakua pointi zote tisa, na kubaki katika nafasi yao ya kwanza kwenye msimamo
wa Ligi, nafasi ambayo walikuwa nayo wakati wanaingia raundi ya 16.
Pia katika raundi hizo tatu
ambapo Simba haikufungwa bao hata moja, Mwanjali alicheza dakika zote 270, na
bila kuonyeshwa kadi yoyote. Alichangia kwa kiasi kikubwa katika mafanikio ya
timu yake huku akiongoza safu ya ulinzi.
Kwa kushinda tuzo hiyo ya
mchezaji bora, Mwanjali atazawadiwa kitita cha sh. 1,000,000 (milioni moja) na
wadhamini wakuu wa Ligi hiyo Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania.
Wachezaji wengine walioshinda
tuzo za mchezaji bora kwa msimu wa 2016/2017 hadi sasa ni John Raphael Bocco wa
Azam (Agosti), Shiza Ramadhan Kichuya wa Simba (Septemba), Simon Happygod Msuva
wa Yanga (Oktoba), na Rifati Hamisi wa Ndanda (Novemba).
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA
WA MIGUU TANZANIA (TFF)
Post a Comment