.png)
Dirisha la usajili kwa timu
zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Ligi Daraja la Kwanza la
StarTimes na Ligi Daraja la Pili msimu wa 2016/2017 lilifungwa saa 6.00 usiku
wa Jumamosi Agosti 6, 2016.
Hadi dirisha linafungwa, timu kadhaa
hazikuwasilisha kabisa usajili wake licha ya kukumbushwa kwa njia mbalimbali na
uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Usajili wa msimu huu ni kama msimu
uliopita kwamba unafanyika kwa njia au mfumo wa mtandao unaoitwa Transfer
Matching System (TMS) ambao (server) yake au chombo chake cha kutunza
kumbukumbu kipo Makao Makuu ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA)
- Uswisi.
Kwa kawaida mfumo huu upo chini ya
FIFA na TFF hutoa taarifa kwa FIFA tarehe ya kufungua dirisha la usajili na
kufunga.
Mfumo huu huhusisha pande tatu
ambazo ni klabu, shirikisho (TFF) na FIFA. Kimsingi kazi ya usajili hufanywa na
klabu ambako inajaza fomu kwa njia ya mtandao na hupakia viambatanisho kama
vile mikataba ya wachezaji na picha za wachezaji.
Zoezi hili hufanywa na Meneja
Usajili wa klabu husika wakati shirikisho hufanya kazi ya kuhakiki na
kuidhinisha tu na FIFA huratibu na kuusimamia mfumo mzima.
Kabla ya kutangaza kufunguliwa kwa
dirisha la usajili hapo Juni 15, 2016 Shirikisho liliandaa kozi ya mafunzo ya
usajili kwa klabu zote 64 zikiwa ni 16 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara; 24
zitakazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza la StarTimes na timu 24 zitakazoshiriki
Ligi Daraja la Pili msimu wa 2016/2017.
Baadhi ya timu hazikutuma
wawakilishi, lakini ziko zilizofanya jitihada za kuomba usaidizi kwa kufika
ofisini TFF kuomba usaidizi wa kufanya usajili na zilifanikiwa. Kwa Young
Africans, licha ya kuwa hapa Dar es Salaam, haikuomba usaidizi wowote na hata
walipokumbushwa kuhusu suala la usajili, hawakujibu kitu.
Young Africans ambao ni mabingwa wa
Ligi Kuu Tanzania Bara mara mbili mfululizo msimu wa 2014/2015 na 2015/2016, ni
moja ya vilabu ambavyo havikutuma mwakilishi kwenye kozi iliyofanyika Uwanja wa
Taifa kwa siku tatu mfululizo ikigusa wawakilishi wa madaraja ya Ligi Kuu, Ligi
Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili.
Meneja wa TMS wa Young Africans ni
Katibu Mkuu hakuwahi kupata mafunzo ya TMS.
Hivyo sasa klabu zote ambazo
hakuzituma usajili wake, hazina budi kuandaa utetezi utakaokwenda TFF ambao
utatumwa FIFA yenye mamlaka ya kufungua dirisha, na utetezi huo ukikataliwa
timu husika inabidi ishuke daraja ambalo halimo kwenye usajili wa mfumo wa TMS.
TFF kwa sasa inasuburi barua ya utetezi wa klabu ambazo
hazikukamilisha zoezi la usajili ili iutume FIFA. Sambamba na hilo TFF
inatathimini mwenendo mzima kisha itatoa taarifa kwa FIFA ili kuangalia namna
gani ya kushughulikia maeneo yaliyokuwa na upungufu kwa sasa na baadaye.
Post a Comment